WAZIRI SILAA ATATUA MIGOGORO MKOANI MOROGORO

Описание к видео WAZIRI SILAA ATATUA MIGOGORO MKOANI MOROGORO

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa (MB) ametatua migogoro ya Ardhi ya muda mrefu likiwemo eneo la Msitu wa kuni - CCT baada ya wananchi  kuvamia eneo hilo na kuweka makazi yao ya kudumu ambapo Rais  Dkt. Samia Suluhu Hassani alitoa maelekezo juu ya kupimwa eneo hilo na kuwapatia wananchi umiliki halali.

Makubaliano hayo yamefikiwa Julai 9, mwaka huu baada ya Waziri Jerry Silaa kuwasili Wilayani Mvomero na kufanya mkutano na  wananchi waliovamia  eneo hilo.

Akibainisha zaidi katika mgogoro huo wa Msitu wa kuni Waziri Silaa amesema, Dkt. Samia Suluhuhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameelekeza kutoa Ekari 5113 kutoka katika msitu huo na kupima Viwanja 1204 ambavyo wananchi waliokuwa wakiishi humo watahakikiwa na kupewa hati za umiliki.

"... Rais Samia kaagiza ekari 5113 zimegwe kwenye msitu wa Watanzania na eneo hilo lipimwe viwanja 1204 na hivyo viwanja vitatolewa vibali kwa utaratibu mzuri uliopangwa..." amesema Mhe. Jerry Silaa.

Katika hatua nyingine, Waziri Jerry Silaa amesema Serikali imeridhia kutoa hati miliki za ardhi kwa wananchi walipatiwa maeneo eneo la Msamvu tangu 1978 na kuanzisha makazi ya kudumu na biashara licha ya ramani ya awali iliyoonesha eneo hilo lilitengwa kwa ajili ya  shughuli nyingine za kijamii ikiwemo viwanja vya michezo.

Pia amesema kwa sasa serikali haitatoa vibali vya kumilikisha maeneo ya wazi bali ramani itabaki kama ilivyo na kutaka watendaji wa sekta ya Ardhi hapa nchini  kuhakikisha maeneo yenye migogoro kusikilizwa na kumalizika ili kuepuka kuiingiza serikali kwenye migogoro isiyo na tija.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amempongeza Waziri Jerry Silaa kwa kutenga muda wake kwa ajili ya kutatua kero za wananchi wa Mkoa wa Morogoro hususan zinazohusu migogoro ya Ardhi.

Hapo awali, Kamishna Msaidizi wa ardhi Mkoa wa Morogoro Bw. Frank John Minzikuntwe amesema Mwaka 2022 Serikali ilitoa maelekezo ya kuwahakiki wananchi waliokuwa wamejenga nyumba zao eneo la Msitu wa kuni na baada ya upimaji wa ekari 5113 vimepatikana viwanja 1204 ambavyo vitapewa hati miliki huku maeneo ya wazi yatabaki serikalini.

Nao wananchi akiwemo Bi. Chiku Ramadhani Mgangu Mkazi wa Mianga ameishukuru Serikali kwa kuendesha zoezi la kupimiwa viwanja na kuhakikiwa maeneo yao na kupewa vibali kwa ajili kupewa hatimiliki.

 

Mwisho.

Комментарии

Информация по комментариям в разработке