SODOMA NA GOMORA: MWANZO WA ADHABU KWA JAMII ILIYOFANYA USHOGA—KISA CHA NABII LUTI (LUT) ALAYHI SALAM
ONYO KWA JAMII ZINAZOPINDUA MAUMBILE.
Katika nyakati za zamani, baada ya Nabii Ibrahim (Abraham) kuhamia katika ardhi ya Sham, Mwenyezi Mungu alimchagua ndugu yake wa kibaba, Nabii Luti (Lut) alayhi salam, awe Mtume kwa watu wa miji ya Sodoma na Gomora. Miji hiyo ilikuwa karibu na Bahari ya Chumvi (Dead Sea), katika eneo linalojulikana leo kama Jordan. Ilikuwa ni miji iliyostawi kwa mali na biashara, lakini mioyo ya watu wake ilikuwa imeharibika vibaya kwa uovu.
Watu hawa walikuwa wamejizamisha katika maovu ambayo hayakuwa yameshawahi kuonekana duniani kabla yao. Walikuwa wakiwadhulumu wasafiri, wakiiba mali zao, na mara nyingine kuwaua. Lakini uovu wao mkubwa zaidi ulikuwa ni kuacha wake zao na kuanza kufanya mapenzi ya jinsia moja—wanaume kwa wanaume. Dhambi hii ilienea waziwazi bila aibu, hadi ikawa jambo la kawaida kabisa katika jamii yao. Watu wakaizoea hali hiyo, kiasi kwamba mwanaume kufanya mapenzi na mwanaume mwenzake hadharani ilikuwa ni jambo la kawaida kwao.
Qur’an Tukufu inasimulia uhalisia huu kwa maneno mazito:
“Na (tulimtuma) Luti alipowaambia watu wake: ‘Je, mnafanya uchafu ambao hakuna mtu yeyote katika walimwengu aliyewatangulia kufanya? Hakika nyinyi mnawaendea wanaume kwa matamanio badala ya wanawake. Bali nyinyi ni watu mliozidi mipaka.’”
(Surat Al-A‘raf 7:80–81)
Nabii Luti hakunyamaza. Alisimama mbele ya jamii iliyooza kimaadili na akaanza kuwaita kwa subira na hekima. Aliwakumbusha kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mola wao, na kwamba njia waliyokuwa nayo ingewapeleka kwenye adhabu kali. Lakini majibu yao yalikuwa ni kejeli, dharau, na vitisho. Walitamka kwa kiburi wakisema:
“Watoeni watu wa Luti katika mji wenu; hakika wao ni watu wanaojitakasa!”
(Surat Al-A‘raf 7:82)
Hata mke wa Nabii Luti hakusimama upande wa haki. Moyo wake ulikuwa pamoja na waovu, na alikuwa akiwasaidia kwa siri dhidi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu. Alikuwa mwanamke aliyewafanyia wanaume mipango na kuwaunganisha katika kufanya mapenzi ya wanaume kwa wanaume.
Siku moja, Mwenyezi Mungu alimtumia Nabii Luti wageni watatu—malaika—waliokuja kwa umbo la vijana wazuri. Luti alipowaona, moyo wake ulijaa huzuni na hofu, akijua tabia ya watu wake. Hakutaka wageni wake waumie mikononi mwa jamii iliyopotea. Qur’an inasema:
“Na walipomjia wajumbe wetu Luti, alisikitika kwa ajili yao, na kifua chake kikawa kifupi kwa sababu yao.”
(Surat Hud 11:77)
Habari za kuwepo kwa wageni hao wazuri ziliposambaa, baada ya mke wa Nabii Luti kutoa siri hiyo, watu wa mji walimiminika nyumbani kwa Luti kwa pupa na tamaa. Luti alijaribu kwa mara ya mwisho kuzuia uovu huu. Aliwaambia kwa sauti ya uchungu na maumivu:
“Hawa ni binti zangu (waoeni), wao ni safi zaidi kwenu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, wala msinivunjie heshima mbele ya wageni wangu.”
(Surat Hud 11:78)
Lakini walijibu kwa dharau, wakisema hawana haja na wanawake, bali wanataka wanaume wenzao.
Hapo ndipo ukweli ulipodhihirika. Malaika walimwambia Luti kuwa wao si wageni wa kawaida, bali ni wajumbe wa Mwenyezi Mungu waliokuja kuitekeleza hukumu Yake. Walimwamuru Nabii Luti (A.S) aondoke usiku pamoja na familia yake na waumini wachache, bila yeyote kati yao kuangalia nyuma.
“Basi ondoka na familia yako sehemu ya usiku, wala asitazame nyuma yeyote miongoni mwenu, isipokuwa mke wako.”
(Surat Hud 11:81)
Alfajiri ilipofika, adhabu ya Mwenyezi Mungu iliteremka kwa namna ya kutisha. Ardhi ilipinduliwa juu chini, sauti kali ikawapiga, na mawe ya udongo uliooka yakawanyeshewa kutoka mbinguni.
“Tukaifanya miji hiyo juu yake chini yake, na tukawanyeshea mawe ya udongo uliooka.”
(Surat Al-Hijr 15:74)
Mke wa Luti, kwa sababu ya usaliti wake na kuangalia nyuma kwa masikitiko juu ya waovu, aliangamia pamoja nao. Mke wa Luti alikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakipigia debe mapenzi ya jinsia moja. Hata walipokuwa wakiondoka katika mji huo ili kupisha adhabu ya Mwenyezi Mungu, yeye hakuridhika, akavunja amri, akageuka nyuma, na kwa usaliti wake akaangamizwa pamoja nao:
“Mke wake alikuwa miongoni mwa waliobaki nyuma.”
(Surat Al-A‘raf 7:83)
Nabii Luti na waliokuwa pamoja naye waliokolewa, huku miji hiyo ikifutwa kabisa katika uso wa ardhi. Mahali pake pakabaki kuwa ni Bahari ya Chumvi—ikiwa ni ishara ya milele kwa wenye kutafakari.
“Hakika katika hayo zipo ishara kwa wenye kufikiri.”
(Surat Al-Hijr 15:75)
Biblia pia ilizungumza hili na inamaandiko ya kutosha kuhusu hili ila me nimenukuu moja;
“Sodoma na Gomora… waliotenda uasherati na kufuata mwili wa namna nyingine, wamewekwa kuwa mfano wa kuadhibiwa kwa moto wa milele.”
(Yuda / Jude 1:7)
Namaanisha kuwa katika hili hakuna kisingizio dini zote zinakataza maandiko ni mengi ila nimeweka machache ambayo yanatosha kueleweka.
Информация по комментариям в разработке