RAIS wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU), licha ya changamoto zinazokikumba chombo hicho cha uongozi tangu kuanzishwa kwake mwaka mmoja uliopita.
Akizungumza bungeni jijini Cape Town katika mjadala wa bajeti ya urais, Ramaphosa amesema ingawa amekumbana na ukosoaji mkali kutoka kwa wabunge kuhusu hali ya uchumi, ongezeko la uhalifu na tuhuma za rushwa, bado anaamini kuwa GNU ni jukwaa muhimu la kushirikiana kwa maslahi ya taifa.
“Kwa kweli, kulikuwa na tofauti na migogoro miongoni mwa wanachama wa GNU, jambo ambalo ni la kawaida. Lakini, licha ya tofauti hizo, washirika wa GNU wamechagua kushirikiana kwa ajili ya manufaa ya wananchi wote wa Afrika Kusini,” amesema Ramaphosa.
Itakumbukwa, Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilianzishwa baada ya uchaguzi mkuu na ni muungano wa vyama mbalimbali, lakini imekuwa ikikumbwa na misuguano ya kiitikadi na kisera. Changamoto kubwa zaidi ilikuwa mwezi Februari mwaka huu, GNU iliposhindwa kupitisha bajeti ya taifa mara mbili ambalo ni tukio la kihistoria kwa taifa hilo.
Mgogoro mkubwa wa sasa uko kati ya vyama vikuu viwili, Chama cha African National Congress (ANC) na Democratic Alliance (DA). Mbunge wa ANC, Khusela Diko, alifichua kuwa DA imegawanyika ndani kwa ndani, ambapo kundi moja linaongozwa na kiongozi wa chama, John Steenhuisen, anayetaka GNU ifanye kazi, na kundi jingine likiongozwa na Helen Zille, mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho, ambaye anaonekana kuwa dhidi ya muundo huo wa serikali.
“DA sasa iko vitani na yenyewe,” amesema Diko, akisisitiza kuwa baadhi ya wanachama wa ANC wanataka DA iondolewe serikalini kwa sababu haiwezi kuwa sehemu ya serikali inayopinga bajeti inayopaswa kuitekeleza.
Ukosoaji mzito kwa Rais
Wakati wa mjadala huo wa bajeti, Rais Ramaphosa alikumbwa na ukosoaji mkali kutoka kwa wabunge wa vyama mbalimbali. Alituhumiwa kuwa ni mfano wa uozo serikalini, kushindwa kukabiliana na rushwa, na kuiacha nchi ikizama kwenye uhalifu na kudhoofika kwa serikali za mitaa.
Mbunge wa DA, Darren Bergman, alihoji urithi wa Ramaphosa, akisema matatizo mengi aliyoyarithi yamezidi kuwa mabaya chini ya utawala wake. Kwa upande wake, Mbunge wa MK, Jaji John Hlophe, naye alikuwa mkosoaji mkali wa serikali ya Ramaphosa.
Hata hivyo, Rais Ramaphosa alitetea mafanikio ya Afrika Kusini tangu kupatikana kwa demokrasia miaka 31 iliyopita, akisema licha ya changamoto nyingi, maisha ya wananchi yameboreshwa kwa kiasi kikubwa, hususan katika upatikanaji wa huduma za msingi kama maji safi.
“Tusikate tamaa na kupoteza matumaini. Tumeanza safari ya mabadiliko, na ingawa bado kuna kazi kubwa mbele yetu, tumepiga hatua katika kuboresha maisha ya wananchi wetu,” alisema Rais.
Ikulu na tume mpa ya uchaguzi
Masuala kuhusu utendaji wa Ikulu pia yalijitokeza, huku wabunge wa EFF wakidai kuwa taasisi hiyo imeoza kuanzia juu na kwamba taifa limekabidhiwa kwa magenge ya kihalifu na madalali wa dawa za kulevya.
Ramaphosa alijibu kwa kusisitiza kuwa Ikulu si taasisi ya utekelezaji wa miradi ya moja kwa moja, bali ni kituo cha kuratibu sera na mikakati ya kitaifa. Alikumbusha kuwa hivi karibuni ameanzisha tume ya uchunguzi kuchunguza madai ya uhalifu na uingiliaji wa kisiasa ndani ya vyombo vya usalama, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kusafisha taasisi za serikali.
Pia alikiri kuwa wananchi wamechoshwa na mipango isiyo na matokeo, na ndiyo maana Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini (DPME) imeanzishwa ili kufuatilia utekelezaji wa sera na mipango ya serikali.
Majadiliano ya Kitaifa yavutia ukosoaji
Mjadala mwingine uliowasha moto ni kuhusu Majadiliano ya Kitaifa (National Dialogue) yanayotarajiwa kugharimu takriban R700 milioni(sawa na sh106.4 bilioni) Baadhi ya wabunge walitangaza kususia mjadala huo, wakipinga gharama kubwa isiyo na msingi.
Lakini kwa upande wake, Rais Ramaphosa alitetea mpango huo, akisisitiza kuwa ni wakati wa kujitathmini kama taifa. “Je, tunataka kuvunja au kujenga upya?” alihoji Rais.
Mjadala huu bungeni umeonesha wazi kuwa safari ya GNU bado ni ndefu na yenye changamoto nyingi, lakini pia umebeba fursa ya mazungumzo ya kitaifa yatakayoweza kuleta mshikamano, iwapo yataendeshwa kwa uaminifu na nia njema.
Информация по комментариям в разработке